Balozi Maina aliyefika ofisini kwa RC Makalla kujitambulisha kufuatia uteuzi wake hivi karibuni, amempongeza Makalla kwa kuendelea kuimarisha usalama na biashara kwenye mpaka wa Namanga, akirejea ziara yake ya hivi karibuni alipotembelea eneo hilo na kuzungumza na wananchi wa Tanzania na Kenya wanaoishi na kufanya biashara katika eneo hilo.
“Sisi na Tanzania hatuna shida yoyoye na ile ziara yako pale Namanga ndiyo imefanya niamue kuja kujitambulisha kwako, ulifanya kazi nzuri sana kusisitiza kuhusu amani na kujiridhisha kuhusu usalama. Ulitoa majibu ya maswali mengi sana ambayo Kenya tulikuwa tunayapokea na mpaka leo tunatumia ile hotuba yako kuwahakikishia wananchi usalama,”amesema Balozi Maina.
Katika mazungumzo yao, RC Makalla ameutaja mpaka huo na Kituo cha pamoja cha forodha Namanga kama kiungo muhimu cha uchumi wa Kenya na Tanzania, akihimiza umuhimu wa kutunza ujirani mwema, kulinda amani na kukuza biashara miongoni mwa wananchi wa pande hizo mbili.
Viongozi hao kadhalika wamekubaliana kuendelea kushirikiana katika kuondoa vikwazo mbalimbali vitakavyojitokeza, wakisema ushirikiano wao huo wa pamoja umedhamiria kusaidia kutekeleza ndoto za wakuu wa nchi za Tanzania na Kenya kuhakikisha wananchi wananufaika kiuchumi na kijamii kupitia mpaka huo kwa kubadilishana bidhaa, huduma na watalii wanaoutumia mpaka huo.

