TUKUBALI KUSHIRIKIANA ILI KUTATUA MIGOGORO YA WAKULIMA NA WAFUGAJI KATIKA KATA YA FUKAYOSI

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mhe. Shaibu Ndemanga, ametoa wito kwa wananchi wa Kata ya Fukayosi, Halmashauri ya Mji wa Bagamoyo, kushirikiana kwa dhati ili kuweza kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji.

Mhe. Ndemanga amesema hayo wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Fukayosi tarehe 26 Januari 2026, akisema kuwa sababu kubwa inayopelekea kuwepo kwa wafugaji wavamizi ni uwepo wa mashamba pori ambayo bado hayajaendelezwa hadi sasa.

Mhe. Ndemanga ameendelea kusisitiza kuwa wao kama Serikali wamejipanga kuhakikisha wanawafahamu wamiliki wa mashamba pori yote pamoja na mipango yao ya kuyaendeleza mashamba hayo.

Aidha, Mhe. Mkuu wa Wilaya amewataka wamiliki wa maeneo hayo kuwa na jukumu la kulinda maeneo yao, lakini pia kuhakikisha maeneo hayo yanaendelezwa kama ambavyo sheria inamtaka mmiliki kufanya maendeleo katika maeneo hayo.

Pia, Mhe. Ndemanga amesema kuwa ipo haja kwa wananchi kuendelea kufuata taratibu za kupokea wageni wanaotaka kuwa wakazi katika maeneo yao ili waweze kujadiliwa na kuchunguzwa kama ni watu wasio na hatia na waliopo salama kuishi katika maeneo hayo. Aidha, Mhe. Mkuu wa Wilaya amepiga marufuku kupokea mtu na kumpa makazi bila kufuata taratibu zinazotakiwa, ili kuepuka migogoro ya wakulima na wafugaji.

Sambamba na hayo, Mkuu wa Wilaya ametoa rai kwa wafugaji kuhakikisha wanarudisha mifugo kwa wamiliki wa mifugo hiyo ili kuepukana na migogoro baina yao na wakulima.

Ziara ya Mhe. Mkuu wa Wilaya katika Kata ya Fukayosi ilikuwa na lengo la kusikiliza kero za wananchi wa kata hiyo pamoja na kuzitafutia ufumbuzi, huku akiweka wazi dhamira yake ya kuhakikisha ataendelea kutatua kero za wananchi na kuendelea kuwatumikia wananchi hao ili kuhakikisha changamoto zote zinazowakabili zinatatuliwa kwa wakati.








Post a Comment

Previous Post Next Post