Na. Iddi Nassoro Rajabu
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome amezindua mradi wa usambazaji wa umeme katika vitongoji vya Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kutekeleza dhamira ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wananchi wote wanafikiwa na huduma ya nishati ya umeme.
Akizungumza wilayani Siha, wakati wa hafla ya uzinduzi, Mhe. Salome amesema kuwa pamoja na umeme kuunganishwa kwenye kaya, Wizara ya Nishati inaendelea kuhakikisha taasisi za umma, hususan shule, zinaunganishwa pia na umeme ili kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
Katika hafla hiyo, Naibu Waziri aliwasha rasmi umeme katika Kitongoji cha Ngare-Nairobi na kueleza kuwa, "tumeanza na kitongoji hiki lakini katika Wilaya ya Siha pekee Serikali inatekeleza mpango wa kuwasha umeme kwa kaya 5,000 ifikapo mwaka 2030. Hadi sasa kaya 3,000 tayari zimeunganishwa na umeme.
" Katika hatua nyingine, Mhe. Salome amesema Tanzania inaendelea kutekeleza kwa kasi Mpango Mahsusi wa kuwafikishia umeme Waafrika Milioni 300 ifikapo mwaka 2030 (Mission 300) ukiwa na lengo la kuhakikisha wananchi wote nchini wanafikiwa na huduma ya umeme ifikapo mwaka 2030. "Kupitia Mpango wa Misheni 300, TANESCO inalenga kuunganishia umeme wananchi 1,700,000 kwa mwaka ambapo Mkoa wa Kilimanjaro pekee unalenga kuunganisha wananchi 12,000 kwa mwaka na hadi sasa zaidi ya wananchi 9,000 tayari wamepata huduma ya umeme mkoani humu."
Amesema Kwa upande wake, Meneja wa TANESCO Mkoa wa Kilimanjaro, Mha. Merry Kabakuzi amesema Wilaya ya Siha ina jumla ya vitongoji 169 ambapo vitongoji 155 tayari vina umeme huku vitongoji 14 vilivyosalia vikiwa katika Mpango wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) awamu ya pili ya ujazilizi wa vitongoji. Ameeleza kuwa maeneo ambayo umeme umefika kwa kiwango kidogo yataendelea kuongezewa mtandao kupitia Mpango Mahsusi wa misheni 300.








