Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Bagamoyo, Mhe. Mohamedi Usinga, leo tarehe 15 Desemba 2025, amefanya ziara ya kutembelea na kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa ndani ya Halmashauri hiyo
Katika ziara hiyo, Mhe. Usinga aliambatana na Diwani wa Kata ya Dunda, Mhe. Amiry Mpwimbwi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira ya Halmashauri ya Mji wa Bagamoyo. Lengo la ziara lilikuwa ni kujionea maendeleo ya utekelezaji wa miradi, kutathmini ubora wa kazi zinazoendelea pamoja na kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa mujibu wa mipango na viwango vilivyowekwa.
Miradi iliyotembelewa ni pamoja na ujenzi wa jengo la watoto njiti katika Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo, mradi unaolenga kuboresha huduma za afya kwa watoto wachanga na kupunguza vifo vitokanavyo na changamoto za huduma za awali. Aidha, viongozi hao walikagua ukarabati wa Soko la Uhindini, unaotarajiwa kuboresha mazingira ya biashara na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wafanyabiashara wa eneo hilo.
Ziara hiyo pia ilihusisha ukaguzi wa ujenzi wa Bagamoyo Plaza, mradi wa kimkakati unaolenga kuchochea ukuaji wa uchumi wa mji wa Bagamoyo, pamoja na ujenzi wa jengo la ofisi za Halmashauri katika eneo la Ukuni, litakaloboresha ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhe. Mwenyekiti wa Halmashauri alisisitiza umuhimu wa usimamizi thabiti wa miradi ya maendeleo na matumizi sahihi ya rasilimali za umma, akieleza kuwa Halmashauri itaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi yote ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kuleta manufaa yaliyokusudiwa kwa wananchi wa Bagamoyo.











