Rais Samia Awatunuku Kamisheni Maafisa Wapya wa JWTZ Monduli

 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amehudhuria na kuongoza sherehe za kutunuku Kamisheni kwa Maafisa Wanafunzi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi (TMA) Monduli, mkoani Arusha, tarehe 22 Novemba 2025.

Mara baada ya kuwasili chuoni hapo, Rais Samia alipokelewa na viongozi mbalimbali na baadaye kusimama wakati Wimbo wa Taifa ukiimbwa kabla ya kuanza kwa ratiba ya shamrashamra za mafunzo na mahafali.

Katika sherehe hizo, Rais Samia alikagua Gwaride rasmi la kumaliza mafunzo ya Maafisa Wanafunzi wa JWTZ, wakiwemo wahitimu wa kundi la 06/22 Shahada ya Sayansi ya Kijeshi, kundi la 72/24–Regular, pamoja na wahitimu wa mahafali ya sita ya Shahada ya Kwanza ya Sayansi ya Kijeshi.

Aidha, Rais Samia aliwatunuku Kamisheni Maafisa Wanafunzi na kuwavisha cheo cha Luteni Usu, ikiwa ni ishara rasmi ya kuingia katika ngazi ya uafisa ndani ya JWTZ. Pia aliwazawadia Maafisa Wanafunzi waliofanya vizuri zaidi katika mafunzo yao.

Katika hatua nyingine, Mhe. Rais alikabidhi vyeti kwa wahitimu 106 wa Shahada ya Kwanza ya Sayansi ya Kijeshi katika mahafali yaliyofanyika sambamba na sherehe hizo. Wahitimu walionekana na furaha tele wakati wakivalishana vyeo na kuungana na ndugu, jamaa na wakufunzi katika kupigwa picha za kumbukumbu.

Sherehe hizo zilipambwa na matukio mbalimbali ya kijeshi na kimahafali, yakionesha nidhamu, umahiri na uwezo wa kiutendaji wa jeshi katika kuandaa viongozi wapya wa kijeshi kwa ajili ya kulitumikia Taifa.



Post a Comment

Previous Post Next Post