Hatua hiyo imeelezwa itachochea kasi ya utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia na kusaidia kufikia lengo la Serikali la kuwa na asilimia 80 ya Watanzania wanaotumia nishati safi ifikapo mwaka 2034.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya maofisa wanaoratibu utekelezaji wa mkakati huo kwa mikoa na Halmashauri za Nyanda za Juu Kusini, yaliyofanyika mkoani Mbeya, Parmet alisema elimu hiyo imekuja kwa wakati muafaka kwani mikoa hiyo inaongoza kwa kilimo na uzalishaji wa mazao ya miti, lakini bado matumizi ya kuni na mkaa ni makubwa.
“Mikoa hii inaongoza kwa kilimo cha miti, lakini pia matumizi ya kuni ni makubwa. Elimu hii itasaidia Maofisa Dawati kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kutumia nishati safi ya kupikia na kuachana na mapishi ya mazoea,” alisema Parmet.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia kutoka Wizara ya Nishati, Benezeth Kabunduguru, alisema mafunzo hayo ni endelevu na yanalenga kuhakikisha kila Ofisa Dawati nchini anapata uelewa wa kina kuhusu nishati safi ya kupikia, ili waweze kuwafikia wananchi kwa urahisi na ufanisi zaidi.
“Tunataka kila Afisa Dawati awe na uelewa wa kina kuhusu nishati safi ya kupikia ili aweze kuwafikia wananchi kwa ufanisi. Lengo letu ni kufikia asilimia 80 ya matumizi ya nishati safi ifikapo mwaka 2034,” alisisitiza Kabunduguru.
![]() |
Ameongeza kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia ni kipaumbele cha taifa na dunia kwa ujumla, kutokana na mchango wake katika kulinda mazingira, kuboresha afya za wananchi na kuinua uchumi wa kaya.
Naye, Ofisa Mwandamizi Mshauri Masuala ya Kiufundi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Deusdedit Malulu, aliwahimiza Maofisa Dawati kutumia mafunzo hayo kutangaza fursa za uwekezaji na ujasiriamali katika sekta ya nishati safi ya kupikia, ikiwemo utengenezaji wa majiko banifu, mkaa mbadala, na miradi ya ruzuku kupitia REA.
“Tunataka kuona maafisa wakitumia mafunzo haya kuhamasisha vijana na vikundi vya wajasiriamali kuanzisha miradi ya nishati safi itakayowanufaisha kiuchumi,” alisema Mhandisi Malulu.
Mafunzo hayo yamehusisha Maafisa Dawati wa Halmashauri na Mikoa ya Mbeya, Iringa, Songwe, Katavi, Rukwa, Njombe na Ruvuma.



