RAIS Samia Suluhu Hassan, amesisitiza juu ya umuhimu wa juhudi za pamoja katika kukuza matumizi ya nishati safi ya kupikia na ajira kwa vijana ili kuhakikisha ustawi wa watu wa kanda hiyo.
Rais Samia amesema hayo Arusha wakati wa maadhimisho ya miaka 25 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) yaliyofanyika jijini Arusha.
Amesema serikali yake itaendelea kusimamia matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kupunguza vifo vinavyotokana na utoaji wa hewa ya kaboni kutoka kwenye mkaa na kuni.
Amesema Tanzania imejiwekea lengo la kuhakikisha ifikapo mwaka 2034, angalau asilimia 80 ya Watanzania watumie nishati safi ya kupikia.
Amesema Tanzania inawekeza katika uzalishaji wa umeme, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Mradi wa Bwawa la Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) utakaozalisha zaidi ya MW 2,000.
Rais Samia amesema juhudi hizo ni sehemu ya kupambana na athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi, kwani Tanzania inapoteza takribani ekari 400,000 za ardhi kila mwaka.
Amesema kutokana na halo, Tanzania inatumia kati ya asilimia nne hadi tano ya pato lake la taifa kupambana na uharibifu wa mazingira.
Naye, Rais Yoweri Museveni wa Uganda amezikumbusha nchi za EAC kuhusu maono ya waasisi wake kama Mwalimu Julius Nyerere, Mzee Jomo Kenyatta na Rais Milton Obote, ambao walikusudia kuunda ushirikiano utakaokuza ustawi wa watu na usalama.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Burundi, Prosper Bazombaza amesisitiza umuhimu wa kuboresha biashara za mipakani kwa kushughulikia vikwazo vya biashara (NTBs).
