ZANZIBAR: Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi, Mhandisi Zena Said amewataka wanaume kwenye maeneo mbalimbali kuwapa ushirikiano wanawake haswa wenye maono makubwa ya kiuchumi na kijamii.
Zena ameyasema hayo usiku wa kuamkia leo katika kilele cha tuzo za Malkia wa nguvu zinazotolewa na Clouds Media Group ambapo Malkia tisa akiwemo mtoto wa Rais Samia na mke wa Rais wa Zanzibar Mariam Mwinyi kushinda tuzo hizo.
Zena amesema wanawake wakiwezeshwa wanaweza na pia kuwataka wanawake wote visiwani Zanzibar kujiunga na majukwaa ya uwezeshaji kiuchumi ili waweze kutambulika na kuunganishwa kwenye fursa mbalimbali zinazopatikana ambazo zitawawezesha kujikwamua kimaisha wao binafsi, familia zao na serikali kwa ujumla.
Tuzo ya Heshima imeenda kwa Mama Mariam, Mke wa Rais wa Zanzibar, muanzilishi wa taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF).
ZMBF imewagusa wanawake wanaojishughulisha na uchumi wa buluu kwa makundi na kuwapatia boti za kisasa zenye mashine, vifaa vya kazi, na tumaini jipya na kubadilisha taswira ya maisha yao.
Pia, kupitia Maisha Bora, Afya Bora, zaidi ya watu 10,000 wanawake, watoto, na wazee wamepata huduma za vipimo na matibabu kutoka kwa madaktari bingwa.
Taasisi hiyo pia imekua ikisimamia masuala ya lishe, elimu jumuishi katika masuala ya kiuchumi, afya na masuala ya unyanyasaji wa kijinsia.
Aidha, Malkia wa nguvu wengine waliopata tuzo ni washindi Ramla Khamis Juma, yeye ameshinda kwenye kipengele cha biashara ya chakula, ni mkazi wa Pemba, kwa sasa ni mpishi mkubwa ambae alianza kupika akiwa mtaani mpaka baadae kuajiriwa Ikulu kama mpishi, lakini bado alikua na ndoto ya kusimamisha biashara yake mwenyewe, kwa sasa amefanikiwa kusimamisha biashara yake na ameajiri zaidi ya wafanyakazi 200.
Mwingine ni Aisha Bakari Mohamed (Hijab Dj) yeye ameshinda tuzo ya Sekta ya Burudani, akiwa Binti mdogo aliyezua gumzo kwa kuonekana DJ anayepiga muziki bila kuonyesha maungo yake, yeye ni hijab mwanzo mwisho, Kwa sasa umaarufu wake si Zanzibar pekee ni mpaka nje ya Zanzibar anapata mialiko ya kwenda kupiga muziki.
Mshindi Mwingine ni Saida Abdallah Mohamed, aliyeshinda tuzo ya Sekta ya Viwanda kupitia biashara ya viungo mbalimbali vya Chakula, ameifanya kazi hiyo kwa miaka 10 sasa.
Sekta ya Ujasiriamali Bora Tuzo imeenda kwa watu wawili, wa kwanza ni Fatma Eliah Masimba aliyeanza kuwa mhudumu wa Mapokezi wa Hotel baadae akawa mmiliki mwakilishi, kwa sasa yeye ni Mkurugenzi katika biashara kubwa ya familia yake.
Akiwa mfanyakazi wa hoteli alikutana na Mume wake, Safari ya ujasiriamali na bishara imeendelea wakiwa wawili na kwa sasa anasimimamia bishara mbalimbali ikiwa ni pamoja na vituo vya mafuta, ujenzi na usafirishaji.
Ujasiriamali tuzo nyingine imeenda kwa Fatma Salum Abdalah (Bi Sufa), yeye aliozeshwa akiwa na miaka 14 mara baada ya kuhitimu elimu ya msingi, baadae matokeo yalitoka akawa amefaulu hivyo akaendelea na masomo.
Alipomaliza shule, alianza maisha yake ya ujasiriamali na bishara nyingi katikati ya changamoto. Kutokana na maisha yake kutopata msingi mzuri wa kusoma aliamua kuanzisha shule na kuziita Sufa Schools ambazo zipo kwa zaidi ya miongo miwili, mbali na shule ni mmiliki wa store kubwa ya vitu vya jumla, frame za kupangisha na mkulima mkubwa kutokana na mashamba aliyonayo.
Sekta ya Utalii, Mshindi ni Mafunda Kombo Faki ambae ni mwanzilishi na mkurugenzi wa ZanVacay. Kupitia ZanVacay, sio tu kwenye eneo la utalii linalohitaji kuongezewa thamani, ZanVacay imemtambulisha Mafunda katika ulimwengu wa kukutana na vijana, kutoa mafunzo mbalimbali yanayohusisha uongezaji wa thamani, pamoja na kuwa mmiliki wa ZanVacay, ni mwajiriwa katika shirika la bima, na ni mshereheshaji katika matukio mbalimbali.

