Mwinjuma: “Ladies First” vipaji vipya vitaibuliwa

 

Na mwandishi wetu : Iddi Nassoro Rajabu.

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma amesema kuwa, Serikali ina matumaini makubwa kuwa vipaji vipya vitaibuliwa kupitia Mashindano ya Riadha ya Wanawake na kulelewa ili viweze kushiriki mashindano ya kitaifa na kimataifa.

Mwinjuma amesema hayo wakati akifungua mashindano hayo yajulikanayo kama “Ladies First” ambayo ni msimu wake wa saba yanayoendelea kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es salaam leo Novemba 29 2025.

Ameongeza kuwa, mashindano hayo yamekuwa chachu muhimu ya kuandaa wanariadha watakaoiwakilisha nchi katika mashindano mbalimbali ikiwamo Jumuiya ya Madola, Afrika na Olimpiki zijazo.

“Niwapongeze sana JICA, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) kwa kuendesha mashindano haya kwa mafanikio makubwa. Yamekuwa yakifanyika kwa msimu wa saba sasa,” amesema Mwinjuma.

Aidha, Mwinjuma amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika michezo ili kuondoa dhana potofu kuhusu nafasi yao katika sekta hiyo huku akibainisha kuwa, licha ya ushiriki wao kuwa mdogo ukilinganisha na wanaume, timu za wanawake zimeendelea kufanya vizuri.

Post a Comment

Previous Post Next Post