Rais Samia: Ndugulile ameweka heshima Tanzania

 


Rais Samia Suluhu Hassan ameongoza shughuli ya kuuga mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Kigamboni na Mkurugenzi Mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Mheshimiwa Dk Fautine Ndugulile katika viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam.
Akitoa salamu za pole, Rais amesema Dk Ndulile ameweka heshima kwa Tanzania kutokana na nafasi aliyoipata katika Shirika la Afya Duniani (WHO).

Amesema kuondoka kwake ni kugumu lakini hiyo ni mipango ya Mwenyezi Mungu na kutaka Watanzania kulipokea jambo hilo.

“Sisi wanadamu tunapanga lakini Mungu naye anapanga yake, kazi ya Mungu haina makosa, tumshukuru kwa uhai na zawadi ya maisha yake, tutaendelea kumuombea na kuiweka familia yake kwenye maombi.

“Marehemu Dk Ndugulile ameweka heshima katika nchi yetu kwa kupata nafasi WHO, niseme kwamba Mungu amechukua amana yake lakini kwetu sisi ni kuendelea mbele tena kwenye ushindani wa nafasi hiyo,” amesema.

Rais amesema Tanzania itatafuta mgombea mwingine mwenye sifa zinazoweza kushindana na ulimwengu na kuingia tena kwenye ushindani kwa nguvu ile ile ili kuweka heshima ya nchi.

Alisema ni wajibu wa nchi kuhakikisha Watanzania wabobezi wanawekewa nguvu ili waweze kuwakilisha katika fani za kimataifa kama walivyofanya kwa Dk Ndugulile.


“Mheshimiwa Dk. Ndugulile aligombea, Serikali ikamuunga mkono na akapata,hata hivyo Mwenyezi Mungu hakutaka iwe hivyo na leo tunamuaga mwenzetu na hatujui sisi safari yetu ni lini maana tunakuja na kuondoka”, alisema.



Post a Comment

Previous Post Next Post